Lissu: Lowassa ni tembo wa siasaAmesema figisu figisu zote za kisiasa wanazofanyiwa Chadema zinatokana na uwapo wa Waziri Mkuu huyo wa zamani ndani ya chama hicho

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema marufuku ya kisiasa iliyowekwa na Serikali, kwa kiasi kikubwa, imemlenga Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye anamuelezea kuwa ni “tembo wa siasa za Tanzania”.

Lissu alisema katika mahojiano maalum na Mwananchi ofisini kwake wiki iliyopita kwamba walioweka marufuku hiyo wanamuogopa kutokana na mvuto mkubwa alionao kwa wananchi.“Edward Lowassa ni tembo aliyeko katikati ya uwanja wa siasa za Tanzania; ukifumba macho hapotei yupo pale; ukisema hayupo, yupo pale, ana nguvu za kisiasa,” alisema Lissu.

“Marufuku hii ya siasa kwa kiasi kikubwa imelengwa kwa Edward Lowassa. Wanamuogopa. Kwa hiyo, wanaosema Lowassa ni oili chafu, kwa nini wanakimbiakimbia? Kwa nini wanahangaika hivi? Akienda Kariakoo mji mzima unachafuka; akitaka kwenda kwenye mazishi, mji mzima unataharuki; juzi juzi alitaka kwenda kwenye mahafali Muhimbili pakawa hapafai. 

Oili chafu(hiyo)?” Mbunge huyo wa Singida Mashariki alisema Lowassa ni mwanasiasa mwenye nguvu nchini ambaye licha ya kusakamwa sana na wapinzani alipokuwa Waziri Mkuu, hasa alipohusishwa na kashfa ya Richmond na baadaye aliposakamwa na wanachama wa CCM alipohamia Chadema mwaka jana, bado katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 alipata kura milioni 6.07 huku mshindi Rais John Magufuli akijikusanyia kura milioni 8.8.

Lissu alisema juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni kumdhibiti Lowassa kwa sababu anaogopwa. Alisema Chadema walifanya uamuzi sahihi kumpokea Waziri Mkuu huyo wa zamani na kumpa nafasi ya kugombea urais.

Kwenye siasa za kiuchaguzi katika nchi ambazo zimetawaliwa muda mrefu na vile vinavyoitwa vyama vya ukombozi, ili kukiondoa chama cha ukombozi madarakani unahitaji kipasuke, na ili kipasuke inabidi uwe na mtu anayeweza kukipasua,” alisema Lissu.

Mwanasiasa huyo alitoa mifano mbalimbali ya vyama vya ukombozi vilivyoanguka, ukiwemo wa chama cha Kanu nchini Kenya kilipasuka baada ya wanasiasa mahiri kuondoka, kama George Saitoti, Raila Odinga na Rais wa zamani, Mwai Kibaki.

Hata (Mwalimu Julius) Nyerere alisema upinzani wenye nguvu utatoka CCM kwa sababu ni chama dola,” alisema Lissu na kusisitiza kuwa katika mkakati wa kuipasua CCM, ilikuwa lazima Lowassa aondoke.

Akizungumzia jinsi mchakato wa kuipasua CCM na kupata mgombea mwenye nguvu ulivyokuwa ndani ya Chadema, Lissu, ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kabla ya uchaguzi huo chama hicho kilitafuta wataalamu wa kuwapa mbinu za kushinda uchaguzi mkuu.

“Tuliwapa pesa wale wataalamu walifanya kazi na kutuletea majibu… ni hadithi ndefu ila kifupi walisema kati ya wagombea wote, Lowassa anatembea na asilimia 18 ya wapigakura,” alisema.

Katika utafiti ilibainika kuwa suala la ufisadi halikuwa na mashiko kwani lilikuwa jambo la tano, kati ya mambo mengi ambayo Watanzania waliohojiwa, waliyaona ni muhimu katika uchaguzi huo.

“Walitueleza kama hiyo ndiyo ajenda yetu kwa wapigakura wa nchi hii, lilikuwa jambo la tano kwa wananchi. Kama chama tukakaa na kuulizana tutafanyaje na kuna watu wakasema wenzake Lowassa huko CCM hawampendi sana,” alisema.

“Dk Slaa ndiye aliyesema tumtafute Lowassa na kueleza kuwa tutampata kirahisi kupitia kwa Askofu (Josephat) Gwajima. Ndiyo maana Dk Slaa wakati anatukimbia alisema mshenga wa Lowassa kuja Chadema alikuwa Gwajima,” alisema.

Alisema pamoja na mambo mengi ambayo Lowassa amesemwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipotangaza matokeo ya urais alipata kura milioni 6.07.

“Hata umtukane Lowassa namna gani na kumchafua, tambua kuwa asilimia 40 ya Watanzania hawakusikilizi, hawakutusikiliza sisi (Chadema) wala wote waliomsema vibaya wakati wa kampeni. Hata kama humpendi huwezi kumpuuza,” alisisitiza.

Lowassa, aliyekuwa mmoja wa makada waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kupitishwa na CCM, alijiengua kwenye chama hicho Julai mwaka jana baada ya jina lake kuenguliwa, lakini Chadema ikampa fursa ya kugombea urais baada ya kujiunga nayo.

Pia aliungwa mkono na vyama vingine vitatu vilivyokuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Amzungumzia Dk Ackson Alipoulizwa kama wabunge wa Chadema wataendeleza msimamo wao wa kususia vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika Dk Tulia Ackson, Lissu alisema mapambano yataendelea.

Alisema naibu spika huyo amewekwa bungeni na Rais Magufuli kuhakikisha mkuu huyo wa nchi hapati shida kama aliyoipata mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.

“Bunge la sasa ambalo lina idadi kubwa ya wabunge wa upinzani ni butu kuliko Bunge la Tisa kwa sababu linaongozwa kutoka Ikulu. Dk Tulia amewekwa na Ikulu kuongoza Bunge kwa manufaa ya Ikulu…kuhakikisha Bunge haliisumbui Ikulu. Kwa kweli anaifanya kazi aliyotumwa kwa umahiri sana,” alisema.

Alisema uhodari wa kufanya kazi ‘aliyotumwa’ ndiyo sababu ya wabunge mahiri kutokuwapo bungeni baada ya kupewa adhabu mbalimbali na naibu spika huyo.

Katika Bunge la Bajeti lililomalizika mwanzoni mwa Julai, takriban wabunge 10 wa upinzani, akiwamo Lissu walisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa vipindi tofauti kwa kosa la ukiukwaji wa kanuni na kusababisha vurugu bungeni.

“Nimefungiwa vikao 44 wakati kanuni za Bunge zinasema ukifanya kosa la kwanza adhabu yako ni kufungiwa vikao vitano, kosa la pili unafungiwa vikao 10 na kosa la tatu na kuendelea adhabu yako ni kufungiwa vikao 20 na adhabu nyinginezo. Sasa adhabu nyinginezo ni vifungo 44?” alihoji.

“Nimefungiwa mpaka Novemba, nilifungiwa vikao 30 vya Juni, na vikao 14 vya Septemba kwa kosa ambalo kwa mujibu wa kanuni za Bunge adhabu yake ni vikao vitano.”

Alisema wakati anapewa adhabu hiyo, hakuwapo bungeni na kusisitiza lengo la kumfungia kutohudhuria vikao vya chombo hicho cha kutunga sheria, pamoja na wabunge wengine mahiri ni kutoa mwanya kwa Serikali kupitisha miswada kandamizi na yenye maswali mengi kuliko majibu.

Hawa watu siyo wajinga sana maana bungeni inapelekwa miswada ambayo inatakiwa isomwe mara ya pili na kupitishwa. Wanajua mwezi Septemba ningekuwepo bungeni ndiyo maana wameamua kunifungia mpaka Novemba,” alisema.

Kuhusu muswada wa kuanzisha mahakama ya mafisadi, Lissu alisema ulipitishwa haraka wakati akiwa katika adhabu hiyo kwa sababu tangu awali aliwaeleza kuwa mahakama hiyo ipo, si kweli kuwa Rais Magufuli ameianzisha.

“Nilimuuliza (Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison) Mwakyembe  kwenye kamati kama mahakama hii haipo? Nilimtaka awaeleze wajumbe kuwa akina Daniel Yona na Basil Mramba (mawaziri wa zamani) wameshtakiwa katika mahakama ipi?” alihoji.“Tumekuwa na mahakama ya mafisadi tangu mwaka 1984 na ilianzishwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward) Sokoine. Mahakama inaposikilizia kesi zote za Takukuru inakaa kama mahakama ya uhujumu uchumi na kwa lugha ya sasa ni ufisadi.”Lissu: Lowassa ni tembo wa siasa Lissu: Lowassa ni tembo wa siasa Reviewed by on 11:36:00 PM Rating: 5

1 comment:

  1. Hivi Lissu haishiwagi uongo?

    Mara naibu spika hafai, mara demokrasia, mara udikteta, oh mara ukuta palepale... Sasa Lowassa Tembo...hahahahahaaaaaa. Akijakuwa nguchiro wa sisasa na muhula wako utakuwa unamalizikaaa.

    ReplyDelete