Majambazi Yaua Polisi 4 Mbande Dar es Salaam usiku wa Kuamkia Leo

Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa jumla ya askari wake wanne wameuawa usiku wa kuamkia leo baada ya majambazi kuvamia tawi la benki ya CRDB lililopo Mbande, wilayani Temeke, Dar es Salaam.

Akizungumza moja kwa moja kupitia kituo cha Redio One Stereo leo asubuhi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, amesema watu kadhaa wamekamatawa na msako unaendelea ili kuwapata waliotekeleza unyama huo.

Sirro amesema taarifa kutoka eneo la tukio zinaonesha kuwa majambazi hao walikuwa 14 na baada ya kufanya mauaji hao, walivamia kituo cha polisi cha Mbande kisha wakavunja stoo na kuchukua sare ya askari na silaha.

Akielezea namna tukio hilo lilivyotokea, Kamanda Sirro amesema wahalifu hao walitumia mwanya wakati askari wakibadilishana lindo katika taasisi hiyo ya fedha na kuibuka ghafla na kuanza kurusha risasi.

Kwa mujibu wa Sirro, gari la polisi limechakazwa kwa risasi na askari mmoja aliyekuwa lindo alifanikiwa kukimbia na ndiye aliyeweza kutoa taarifa na maelezo ya namna tukio lilivyofanyika.

“Watu kadhaa wamekamatwa na tunaendelea na msako. Tunawataka wakiwa hai au wafu,” amesema Kamanda Sirro huku akiwataka watu kujihadhari na yeyote anayejitambulisha kwao kuwa ni askari bila kuonesha kitambulisho.

Ameendelea kusema kuwa baada ya operesheni ya kukomesha mtandao wa wahalifu kama hao na wengine kukimbilia nchi jirani, masalia wameanza kujikusanya na kutekeleza matukio ya mauaji huku askari wakilengwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba  akimjulia hali Raia aliyejeruhiwa
Waziri Nchemba na Kamanda Sirro wakiwa eneo la tukio
Gari ya Polisi ikiwa imezagaa Risasi
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba anasema tukio limeondoa maisha ya askari wanne na kujeruhi raia wawili.

Majeruhi mmoja anaitwa Ally Chionda ambaye ni mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi karibu na benki ya CRDB ambayo pilisi wamepoteza maisha.

Anadai walikuja majambazi kwenye muda kama wa saa 1:15 usiku wakiwa na pikipiki kama tano na kila pikipiki ilikuwa na watu wawili.

Kulikuwa na watu sita au saba ambao walikuwa wamebeba bunduki.

Walipofika walianza kupiga risasi upande wa eneo la benki na upande wa duka lake.

Bahati mbaya risasi moja ilimpata kwenye mguu wa kushoto ikatokeza na kwenda tena kwenye mguu wa kulia.

Majeruhi anaendelea vizuri na anategemea kufanyiwa x-ray kwa uchunguzi zaidi.
 VIDEO:

Majambazi Yaua Polisi 4 Mbande Dar es Salaam usiku wa Kuamkia Leo Majambazi Yaua Polisi 4 Mbande Dar es Salaam usiku wa Kuamkia Leo Reviewed by on 11:00:00 PM Rating: 5

No comments: