SHIRIKISHO
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema Rais John Magufuli
ameonesha mwanzo mzuri katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini,
baada ya kutangaza kushusha Kodi ya Mshahara (PAYE) kwa asilimia mbili
pamoja na kuahidi kufanyia kazi masuala mengine.
Akihutubia
Taifa juzi kwenye kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambayo
kitaifa iliadhimishwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais
Magufuli alitangaza kushusha PAYE kufikia asilimia tisa kutoka 11 ya
sasa kuanzia mwaka wa fedha ujao wa 2016/2017.
“Napenda
kuwataarifu kuwa serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni
zangu, nimeamua kupunguza kodi ya mapato ya mishahara kutoka asilimia 11
ya sasa hadi asilimia tisa kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017, nikiwa
na matarajio makubwa kuwa wabunge wataipitisha Bajeti yangu
niliyoiwasilisha bungeni,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa na
maelfu ya wafanyakazi waliofurika uwanjani hapo.
Akizungumzia
hotuba hiyo ya Rais, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema jana
kwamba Rais Magufuli ameonesha mwanzo mzuri katika kuboresha maslahi ya
wafanyakazi baada ya kupunguza kodi ya mshahara na pia kutangaza hatua
kadhaa za kushughulikia matatizo yanayolalamikiwa na wafanyakazi hao.
“Magufuli
ni taa ya matumaini. Ameonesha mwanzo mzuri katika kuboresha maslahi ya
wafanyakazi. Tuna hakika kwamba ataendelea na kasi hiyo hasa baada ya
kueleza jinsi ambavyo serikali yake iko tayari kushughulikia masuala
mengine ambayo tulimueleza katika hotuba yetu,” alieleza Mgaya.
Katibu
Mkuu huyo wa Tucta alisema kwa msingi huo huo, shirikisho hilo
litaendelea kumuunga mkono Rais Magufuli katika hatua mbalimbali
anazochukua katika kuongoza nchini, ikiwamo suala la kukabiliana na
watumishi hewa.
“Katika
hili la watumishi hewa, tunaahidi tutamuunga mkono. Kwa sababu
kiuhalisia hakuna watumishi hewa, lakini wapo watu wanaotengeneza
watumishi hewa. Hawa ni wenzetu, wanaweza kuwa wanachama wetu au sio
wanachama wetu. Tutamsaidia katika kuwafichua hawa,” alieleza Mgaya.
Katika
risala ya wafanyakazi nchini iliyosomwa na Katibu Mkuu huyo wa Tucta,
ilisema licha ya kwamba wafanyakazi wamekuwa na kilio cha muda mrefu cha
kulipwa kima cha chini cha mshahara kisichotosheleza kumudu kupanda kwa
gharama za maisha, mshahara huo mdogo umekuwa pia ukitozwa kodi ambayo
alieleza kuwa imekuwa ni ya mazoea kwa serikali kwa sababu ni rahisi
kuikusanya.
“Tuna
imani mzigo huu tuliokuwa tumebebeshwa wafanyakazi wa kulipa kodi kubwa
ya mshahara utapungua. Aidha, tunaamini serikali haitoshindwa kupunguza
kodi ya mishahara kuwa tarakimu moja. “Tunashauri Ofisi ya Msajili wa
Hazina ipewe nafasi kubwa katika kusimamia ipasavyo mashirika ya umma
ili kuongeza na kuchangia Pato la Taifa. Aidha, tunapendekeza kodi
inayokatwa kwenye malipo yatokanayo na Mikataba ya Hali Bora Kazini
iangaliwe upya,” alisema Katibu Mkuu wa Tucta.
Rais
Magufuli alisema kwa kushusha PAYE, atakuwa amewapunguzia wafanyakazi
mzigo mkubwa wa makato katika mishahara yao na ameamua kuanza na jambo
hilo kwanza ili changamoto zilizopo za kiuchumi wazikabili.
Alisema
kwa sasa ameamua kushusha kwanza kodi hiyo, ambayo imekuwa ni mzigo
mkubwa kwa wafanyakazi wengi na baadaye mambo yakiwa mazuri wataangalia
namna ya kupandisha mishahara.
Katika
risala yao, Tucta walizungumzia masuala mengine ikiwamo wageni kufanya
kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania, mifuko ya hifadhi ya jamii
kutolipa fedha kwa wakati na pia kufanya uwekezaji usio na tija,
uboreshaji wa mazingira ya kazi, serikali kuhamia Dodoma na wafanyakazi
kuzuiwa kuunda vyama vya wafanyakazi.
Katibu Mkuu wa TUCTA Nicholas Mgaya
Akijibu
hoja ya serikali kuhamia Dodoma, Rais Magufuli alisema tayari yeye
kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
wameshahamia Dodoma na hata yeye huenda Dodoma na kukaa Ikulu ya
Chamwino.
Alisisitiza
nia ya serikali kuhamia Dodoma iko pale pale, hasa kwa kuwa suala hilo
limeelezwa bayana katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, lakini akasema ni
vyema wale wote ambao wanataka serikali kuhamia Dodoma wakaonesha mfano
kwa vitendo ili na serikali nayo sasa iige mfano huo na kuhamia Dodoma.
Kuhusu
hifadhi ya jamii, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imelenga katika
kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafaidika na mfumo wa hifadhi ya
jamii nchini kuliko ilivyo sasa kwa kutaka wananchi wengi zaidi
wanajiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NIHF) ili wawe na uhakika
wa matibabu.
Alisema
serikali inaendelea na juhudi za kupanuia wigo wa huduma za Mfuko wa
Afya Jamii (CHF) na pia kuwawezesha wafanyakazi wengi wa sekta binafsi
kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Lakini
alisema wameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuachana na uwekezaji usio
na tija na badala yake kuangalia uwekezaji wenye manufaa kama kuanzisha
viwanda ambavyo vitaajiri watu wengi na wao kupata wanachama.
Rais
alisema ombi la Tucta juu ya kupunguza mifuko ya hifadhi ya jamii na
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima wamelipokea na kuahidi kulifanyika
kazi katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao 2016/2017 unaoanza Julai
mosi.
TUCTA: Magufuli ni taa ya matumaini
Reviewed by
on
11:00:00 PM
Rating:
No comments: